1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasudani wamenasa kwenye ukatili, njaa na maradhi

Mohammed Khelef
16 Mei 2024

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinaadamu inasema raia nchini Sudan wamenasa kwenye ukatili usioelezeka unaosababishwa na mapigano huku janga la njaa na maradhi yakichanganyika na maafa hayo.

https://p.dw.com/p/4fuuF
Darfur Sudan
Mama na mtoto wake kwenye jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan, akiwa amekimbia mapigano kati ya makundi yenye silaha.Picha: Albert Gonzalez Faran/Unamid/Han/dpa/picture alliance

Afisa wa ngazi za juu wa ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa, Clementine Nkweta-Salami, aliwaambia waandishi wa habari jijini New York siku ya Jumatano (Mei 15) kwamba ukatili wa kutisha unatendwa kwa raia wasiokuwa na hatia.

Msemaji huyo alisema kuna ripoti za ubakaji, mateso na mauaji yenye misingi ya kikabila.

Soma zaidi: Nani anawaunga mkono makamanda wanaoipigania mamalaka Sudan?

"Familia kadhaa zimeparaganyika baada ya watu wapatao miloni tisa kulazimika kuyakimbia makaazi yao, ambayo ni idadi kubwa kabisa ya wakimbizi wa ndani ulimwenguni," alisema.

Mapema mwezi huu, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa  lilizionya pande zinazonpigana nchini Sudan kwamba kuna hatari kubwa ya vifo vinavyotokana na njaa ndani ya jimbo la Darfur na pia maeneo mengine ya nchi hiyoo, endapo hawakuruhusu misaada kulifikia eneo zima la magharibi mwa nchi.

Kauli hiyo ilirejelewa pia kwenye mkutano wa jana kati ya Nkweta-Salami na waandishi wa habari.

RSF na udhibiti wa Darfur

Sudan ilitumbukia kwenye mgogoro mwezi Aprili 2023, baada ya pande zinazowaunga mkono mahasimu wawili wakuu, mkuu wa majeshi Jenerali Abdel-Fattah Al Burhan, kamanda wa Kikosi cha Dharura (RSF), Mohammed Hamdan Dagalo, kuanza vita vya kuwania udhibiti wa mji mkuu, Khatroum.

Sudan | Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo
Mahasimu wa Sudan: kushoto ni kamanda wa kikosi cha RSF, Mohammed Hamdan Dagalo, kulia ni mkuu wa majeshi, Jenereli Abdel Fattah Abdel-Rahman al-Burhan.Picha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Tangu hapo, mapigano yamesambaa kwenye maeneo mengine ya nchi, hasa mijini na jimbo la magharibi la Darfur, na  Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu 14,000 wameshauwa na wengine 33,000 kujeruhiwa.

Soma zaidi: UN: Nusu ya raia wa Sudan wanahitaji msaada wa kiutu

Kwa sasa, wapiganaji wa RSF wametwaa udhibiti wa sehemu kubwa ya Darfur na wameweka mzingiro dhidi ya mji wa El-Fasher, ambao ni mji mkuu wa Darfur Kaskazini, na ambao ndio pekee uliosalia nje ya udhibiti wao. 

Kwa mujibu wa Nkweta-Salami, mapigano makali yalishuhudiwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye mji huo wenye wakaazi 800,000 na kusababisha vifo kadhaa na kuwakimbiza watu kutoka makaazi yao.

"Zimebakia wiki sita tu kabla ya kuanza kwa msimu wa uhaba wa chakula, ambao unasadifiana na msimu wa mvua kubwa na hivyo kuifanya kazi ya kuwafikia watu wenye mahitaji kubwa ngumu," alisisitiza.

Wafadhili hawajatowa fedha kamili

Katikati ya mwezi Aprili, wafadhili waliahidi msaada wa dola bilioni 2.1 kati ya bilioni 2.7 zilizoombwa na Umoja wa Mataifa, lakini kwa mujibu wa Nkweta-Salami "kufikia sasa zimetolewa asilimia 12 tu ya kiwango hicho", hali inayoonesha kwamba wanaweza kushindwa kukabilia na baa la njaa kwa wakati unaostahiki.

Vurugu zauwa watu 38 El-Fashir Sudan

Msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, Leni Kinzli, alisema mwanzoni mwa mwezi Mei kwamba kufikia mwezi Disemba tayari watu wapatao milioni 1.7 kwenye jimbo la Darfur walishakuwa kwenye hali ya dharura ya kuhitaji chakula haraka iwezekanavyo, na sasa idadi hiyo imeshakuwa kubwa zaidi.

Soma zaidi: UN: Miezi sita ya mapigano nchini Sudan yasababisha vifo vya takriban watu 9,000

Kinzli alisema watu wanalazimika kula majani na maganda ya njugu, na endapo msaada haukufika haraka, basi kuna uwezekano wa kushuhudia hivi karibuni vifo vingi vinavyotokana na njaa ndani ya Darfur na maeneo mengine yaliyoathiriwa na vita nchini Sudan.

Vyanzo: AFP, AP